MAKAMU WA PILI WA RAIS AWAFARIJI WANANCHI WALIOPATA AJALI YA BUS ILIOTOKEA MKOANI SHINYANGA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa amesema serikali itaendelea kuwahudumua majeruhi waliopata ajali Mkoani Shinyanga ilitokea tarehe 02, Juni mwaka huu.

Mhe. Hemed alieleza hayo jana alipofika katika Hospital ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salam kuwajulia hali majeruhi hao pamoja na kuwafariji.

Alisema serikali zote mbili zitaendelea kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha afya za majeruhi hao ambao ni watumishi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar waliokuwa ni wanafunzi  wa Kada ya Afya katika chuo cha BUGEMA UNIVERSITY  nchini Uganda.

Makamu wa Pili wa Rais aliwataka madaktari hospitalini hapo kuendelea kuwapatia huduma bora majeruhi hao na serikali ya mapinduzi Zanzibar kupitia mratibu wake anaesimamia shughuli za serilikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili Wa Raisi Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi aliopo Dar es salam ataendelea kutoa ushirikiano unaohitajika.

Aidha, amewaagiza madaktari wanaowasimamia majeruhi kutofanya haraka ya kuwatoa wagonjwa mpaka pale watakapojiridhisha kuwa afya zao zimeimarika na serikali itaendelea  kugharamia matibabu yao.

Alisema serikali ya mapinduzi Zanzibar imefarajika na jitihada zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na madktari katika kuhakikisha Afya za wagongwa zinaimarika siku hadi siku.

Nae Daktari  Bingwa wa masuala ya Mifupa katika hospital ya Taifa Muhimbili  Dk. Victoria Munthali  alimuahidi Mkamu wa Pili wa Rais kuwa  uongozi wa Hospital kwa kushirikana na madktari watendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa mpaka pale Afya zao zitakapotengemaa sawa sawa.

Kwa  upande wao majeruhi wanaopata matibabu katika hospitali ya Taifa Muhimbili walimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa wanamshukuru sana  Mhe. Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi pamoja na wasaidizi wake kwa ushirikiano waliowapatia tangu kutokea kwa ajali hadi sasa.